Moduli hii inalenga kumpa mwanafunzi uelewa wa kina katika nyanja za Isimu Linganishi na Anthropolojia ya Kiswahili. Hivyo, moduli hii inakusudia kumwezesha mwanafunzi kukuza umahiri wa kulinganisha, kulinganua na kuchambua lugha za Kibantu kwa kuzingatia vipengele vya kimuundo, kiuamilifu na kiutamaduni.
Aidha, kupitia mbinu za isimu historia linganishi, mwanafunzi ataendeleza uwezo wake wa kiisimu kwa kuchunguza asili, maendeleo na miundo ya Kiswahili. Katika mchakato huu, ataweza kulinganisha Kiswahili na lugha nyingine za Kibantu, hususan Kinyarwanda, ili kuimarisha maarifa na stadi zake za uchambuzi na matumizi ya lugha katika ufundishaji wa Kiswahili katika miktadha mbalimbali ya kielimu.
Kwa msingi huo, moduli hii itamwezesha mwanafunzi kuchunguza kwa kina na kufafanua uhusiano uliopo kati ya lugha na utamaduni, na hivyo kuimarisha uelewa wa matumizi ya lugha katika mazingira tofauti ya kijamii na kitaaluma.
Moduli hii yenye anwani ya "Uhakiki wa Kifasihi, Elimumitindo na Uandishi wa Bunilizi" ina sehemu kuu mbili. Sehemu ya kwanza inahusiana na nadharia za uhakiki wa fasihi na sehemu ya pili inahusiana na uandishi wa bunilizi.
Katika sehemu ya kwanza, moduli hii inajikita katika kutalii maana ya nadharia, sifa za nadharia, maana ya nadharia za uhakiki na tofauti yake na nadharia ya fasihi na uhakiki. Dhana muhimu kama vile mhakiki na uhakiki zinashughulikiwa pia. Aidha, nadharia za uhakiki zinagawanywa kwa namna zinavyohusiana katika makundi makuu manne. Kila nadharia iliyopo kwa kila kundi inafafanuliwa huku mihimili yake ikiwekwa bayana. Mkaza unawekwa katika kumfundisha mwanafunzi namna ya kuzitumia nadharia katika kufanya uhakiki. Katika sehemu hii ya kwanza, pia kuna mada nyingine zinzohusiana na fasihi ya watoto na fasihi linganishi.
Sehemu ya pili inamakinika zaidi na ujifunzaji wa utunzi wa kazi za kubuni au bunilizi kama taaluma. Hivyo, inaoneshwa ni kwa namna gani mtu anaweza kujifunza bunilizi na kuepuka mtazamo potofu kuwa watunzi wa bunilizi ni wale tu waliozaliwa wakiwa na vipaji. Katika sehemu hii, suala pia la uandishi mzuri linapewa kipaumbele. Hii inafanyika kwa kuweka mkazo katika mambo mawili: uandishi sahihi na uzingatiaji wa wa kiwango cha juu cha usanifu.
Kwa hakika, moduli hii inaweka mkazo zaidi katika nadharia na vitendo. Maarifa pasipo kujua namna ya kuyatumia hayana maana yeyote katika dunia ya sasa.